Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s.) –ABNA– Kamanda wa Makao Makuu ya Pamoja ya Ulinzi wa Anga nchini Iran, Brigedia Jenerali Alireza Elhami, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kusasisha vifaa na mitaala ya mafunzo ili kuendana na mabadiliko katika aina za vitisho vya anga na maendeleo ya teknolojia za kijeshi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRNA), Brigedia Jenerali Elhami ameyasema hayo Jumatatu wakati alipowatembelea wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ulinzi wa Anga cha Khatam al-Anbiya (s.a.w.) katika kambi yao ya milimani.
Amesema Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran kinaandaa mipango ya kuimarisha uwezo na vifaa, pamoja na kusasisha mitaala ya mafunzo, ili maafisa wa baadaye waweze kulinda anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuzingatia aina na mbinu za vitisho vinavyoweza kujitokeza katika siku zijazo.
Brigedia Jenerali Elhami amesema imani na matumaini ya wananchi kwa wana wao waliopo katika Majeshi ya Iran yanaongeza zaidi majukumu na wajibu wa ulinzi wa taifa.
Aidha, amesema uwepo wa vijana wa Iran wenye imani, ari na vipaji, pamoja na kuzingatia elimu, malezi na mafunzo, na kutumia uzoefu muhimu uliopatikana katika vita viwili vya hivi karibuni, umechangia kuimarisha uwezo, ari na utayari wa kijeshi wa walinzi wa anga ya Iran.
Akizungumza na wanafunzi hao wakati wa kuwakumbuka mashahidi wa Ulinzi wa Anga waliokataa kuondoka katika vituo vyao na mifumo ya ulinzi licha ya mashambulizi makali ya maadui, Brigedia Jenerali Elhami amesema ushujaa wao ni historia ya fahari kwa vizazi vijavyo na ni ushahidi wa kimataifa wa uwezo wa taifa kubwa lililosimama kwa nguvu dhidi ya kile alichokiita ubeberu wa dunia.
Amewataka vijana hao wa kimapinduzi kutumia fursa ya malezi na mafunzo waliyonayo ili kulinda nafasi ya juu ya Iran katika ulimwengu, huku wakiendeleza njia ya mashahidi kwa kudumisha roho ya kujitolea na kuongeza juhudi katika kujifunza sayansi na taaluma maalumu.
Kwa kumalizia, Brigedia Jenerali Elhami amesema kuwa kwa kutegemea hazina kubwa ya imani ya wananchi, pamoja na umoja katika itikadi na misingi, Iran itaweza kushinda changamoto na vikwazo vyote.
Maoni yako